Mnamo mwaka 2006, kiasi cha mafuta kwa ajili ya biashara kilithibitishwa kuwepo katika bonde la Ziwa Albert nchini Uganda. Makampuni ya mafuta nchini Uganda; CNOOC LTD, TOTAL na TULLOW PLC yamekamilisha awamu ya utafutaji. Mnamo mwezi Novemba 2020 kampuni ya Total ilikamilisha manunuzi ya hisa zote za kampuni ya Tullow katika uendelezaji wa mradi wa ziwa Albert nchini Uganda ikiwemo Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki na kupelekea kampuni ya Total kuwa mwanahisa mkuu. Makampuni ya Total na CNOOC yanaelekea kwenye hatua ya uendelezaji, ambayo hatimaye itapelekea uzalishaji wa rasilimali za mafuta nchini Uganda.
Mara baada ya kuzalishwa, kiasi cha mafuta ghafi kitachakatwa na kusafishwa nchini Uganda kwa ajili ya kusambazwa katika soko la ndani na kiasi kingene kwenye soko la kimataifa. Uuzaji wa kwenye soko la kimataifa utafanywa kupitia bomba la mafuta; Bomba la Mafuta la Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Bomba hili litajengwa na kuendeshwa na Kampuni ya Bomba la Mafuta ikiwa ni ubia wa Kampuni ya Mafuta ya Uganda (UNOC), Shirika la Maendeleo la Petroli la Tanzania(TPDC) na Kampuni mbili za mafuta, TOTAL na CNOOC.
Mradi wa EACOP
EACOP ni mradi wa bomba la mafuta ghafi yatakayo safirishwa katika soko la kimataifa. Bomba hili lina urefu wa kilometa 1,443 ambalo litasafirisha mafuta ghafi ya Uganda kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani karibu na bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Njia ya bomba la mafuta ilichaguliwa na Serikali ya Uganda kwa kuwa ina gharama nafuu zaidi.
Kutokana na hali ya mafuta ya Uganda, bomba litatakiwa kuwa na joto kutoka mwanzo hadi mwisho. Hii inafanya mradi huu wa bomba la mafuta ghafi (EACOP), kuwa bomba refu zaidi duniani lenye joto.
Bomba litafukiwa ardhini ili kupunguza athari kwenye mazingira, kutakuwa pia na mitambo juu ya ardhi, itakayowekwa ili kupunguza athari za kimazingira na kijamii.
Mradi utazingatia sheria za kitaifa za Uganda na Tanzania na sheria za kimataifa. Kituo cha Kuhifadhi Mafuta cha Baharini na mitambo ya kutolea mafuta itakuwa iko kaskazini mwa bandari ya Tanga kwenye rasi ya Chongoleani.